
Episode #26
Je, Utiifu Wako Utastahimili Mafanikio?
️ Leo kwenye Neno la Leo Leo kupitia 1 Samweli 12:14–15 tunakutana na Israeli katika hatua mpya. Wamepata kile walichosisitiza kukitaka, sasa wana mfalme. Lakini Samweli anawakumbusha kwamba mazingira yao mapya hayajabadilisha jambo la msingi: bado wanapaswa kumcha Bwana, kumtumikia na kuitii sauti yake. Neno la leo linatufanya tujiulize swali ambalo mara nyingi hatujiulizi: Je, utiifu wetu kwa Mungu unaweza kustahimili mafanikio? Ni rahisi kumtafuta Mungu tunapohitaji kazi, tunapotafuta mwenza, tunapoanzisha biashara au tunaposubiri mlango fulani ufunguke. Lakini nini kinatokea baada ya kupata kile tulichokuwa tunakiombea? Je, bado tunaomba? Bado tunasikiliza? Bado tunamtii Mungu? Israeli walikuwa wameingia katika msimu mpya lakini Mungu hakubadilika. Vivyo hivyo hakuna mafanikio, cheo, fedha, ndoa au hatua mpya inayotufikisha mahali ambapo hatuhitaji tena kumtii Mungu. Kwa kweli kadiri tunavyopewa zaidi ndivyo tunavyohitaji kuwa makini zaidi tusije tukaanza kutegemea tulichopewa kuliko Yule aliyetupa. Kwa hiyo leo tujiulize: Je, tunamtaka Mungu mpaka tupate tunachotaka au tutabaki waaminifu kwake hata baada ya kupata tulichokuwa tunakiomba? Mwanzo mzuri ni muhimu lakini Mungu anatuita kwenye utiifu unaodumu katika kila majira, wakati wa uhitaji na wakati wa mafanikio. Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. ✨






