Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
05 OKTOBA 2026
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Wiki iliyopita katika Ofisi ya Kenya ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo, KALRO iliyoko jijini Nairobi nchini Kenya, FAO nchini Kenya kwa kushirikiana na serikali walizindua mradi wa SoilFer. Mradi huu unahusisha kuwa na ramani ya aina za udongo za taifa hilo la Afrika Mashariki ili kusaidia wakulima kuongeza tija kwenye kilimo. Je ina maana gani? Na kwa nini hasa? Stella Vuzo wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa, UNIS- Kenya alizungumza na Barack Okoba, Afisa Programu FAO, Kenya anayeanza kwa kufafanua kilichofanyika siku hiyo. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na jifunze Kiswahili. • Leo ni siku ya kimataifa ya makazi duniani na mwaka huu kauli mbiu ni Makazi bora kwa wote, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-Habitat Anacláudia Rossbach, amesema makazi yanapaswa kuchukuliwa kama kipaumbele cha umma sambamba na ardhi na huduma za msingi, huku uwekezaji zaidi ukielekezwa katika jamii na ushirikiano ukiimarishwa katika ngazi mbalimbali za serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia. Rossbach amesisitiza kuwa takwimu pekee zinaweza zisielezee kwa kina janga la makazi kwani..“familia inaweza kuwa na nyumba, lakini bado wanatumia fedha nyingi kwa pango na wakabakia na fedha kidogo sana kwa ajili ya chakula, elimu na afya. Nyumba inaweza kuwa bei nafuu lakini iko mbali na mahala pa kazi, shule au usafiri.” • Leo pia ni Siku ya Walimu Duniani, ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO limetoa wito wa kuimarisha hadhi na mazingira ya kazi kwa walimu milioni 107 duniani. UNESCO inasema takwimu mpya zinaonesha kuwa katika nchi mbili kati ya kila tano zilizochambuliwa, walimu wanalipwa mishahara midogo kuliko wataalamu wengine wenye sifa zinazolingana, hali inayofanya iwe vigumu kuvutia walimu wapya na kuwaendeleza waliopo katika taaluma hiyo. • Na tukimalizia na masuala ya ulinzi na usalama wa dunia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres usiku wa kuamkia leo amesafiri kutoka Marekani kwenda nchini Pakistan. Pamoja na mambo mengine atakayo fanya nchini humo ziara hii, Guterres atazungumza na viongozi wa Pakistan ambao ni kiungo muhimu cha mazungumzo ya kidiplomasia baina ya Iran na Marekani nchi ambazo zipo kwenye mzozo ambao umeathiri mustakabali wa ulimwengu hususan kwenye kupanda kwa gharama za vitu mbalimbali sababu ya vita baina ya nchi hizo. • Katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili huko Zanzibar, BAKIZA anafafanua maana ya neno, MAFAMBA. Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!